58.Suuratul Al Mujaadalah |
Imeshuka Madina | Ina aya 22 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. MWENYEZI MUNGU amekwisha sikia usemi wa mwanamke anaye jadiliana
nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia
majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
1
2. Wale miongoni mwenu wanao watenga wake zao, hao si mama zao. Hawakuwa
mama zao ila wale walio wazaa. Na hakika hao wanasema neno linalo chusha,
na la uwongo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kusamehe.
2
3. Na wale wanao jitenga na wake zao, kisha wakarudia katika yale
waliyo yasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa maonyo
kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu anayajua yote mnayo yatenda.
3
4. Na asiye pata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi miwili mfululizo
kabla hawajagusana. Na asiye weza hayo basi awalishe masikini sitini. Hayo
ni hivyo ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ndiyo mipaka
ya Mwenyezi Mungu. Na kwa makafiri iko adhabu chungu.
4
5. Hakika wanao pinzana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, watadhalilishwa
kama walivyo dhalilishwa wale walio kuwa kabla yao. Na tulikwisha teremsha
Ishara zilizo wazi. Na makafiri watapata adhabu ya kufedhehesha.
5
6. Siku atapo wafufua Mwenyezi Mungu, na awaambie yale waliyo yatenda.
Mwenyezi Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kushuhudia kila kitu.
6
7. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu
na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa
ni wane wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache
kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale
walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
7
8. Kwani huwaoni wale walio katazwa kunong'onezana kisha wakayarudia
yale yale waliyo katazwa, na wakanong'ona juu ya mambo ya dhambi, na ya
uadui, na ya kumuasi Mtume? Na wakikujia hukuamkia sivyo anavyo kuamkia
Mwenyezi Mungu. Na husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi hatuadhibu kwa
haya tuyasemayo? Basi Jahannamu itawatosha; wataingia humo! Na hayo ndiyo
marejeo maovu yaliyoje!
8
9. Enyi mlio amini! Mnapo nong'ona msinong'one kwa sababu ya mambo
ya madhambi, na uadui, na kumuasi Mtume. Bali nong'onezane kwa kutenda
mema na kuacha maovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa
nyote.
9
10. Kwa hakika minong'ono hiyo inatokana na Shetani ili awahuzunishe
walio amini, na wala haitawadhuru chochote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Na juu ya Mwenyezi Mungu tu ndio wategemee Waumini.
10
11. Enyi mlio amini! Mkiambiwa: Fanyeni nafasi katika mabaraza, basi
fanyeni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi. Na mkiambiwa:
Ondokeni, basi ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni
mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari
za mnayo yatenda.
11
12. Enyi mlio amini! Mnapo sema siri na Mtume, basi tangulizeni sadaka
kabla ya kusemezana kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi zaidi. Na ikiwa
hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
12
13. Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kusemezana kwenu?
Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi shikeni
Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi
Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
13
14. Huwaoni wale walio fanya urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu
amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa
uwongo, na hali kuwa wanajua.
14
15. Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyo kuwa
wakiyatenda ni maovu kabisa.
15
16. Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi
Mungu. Basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.
16
17. Hayatawafaa kitu mali yao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu milele.
17
18. Siku atakayo wafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuwapie kama wanavyo
kuwapieni nyinyi. Na watadhani kuwa wamepata kitu! Kwa hakika hao ndio
waongo.
18
19. Shetani amewatawala na akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Hao ndio kundi la Shetani. Kweli hakika kundi la Shetani ndilo lenye kukhasirika.
19
20. Hakika wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio miongoni
mwa madhalili wa mwisho.
20
21. Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.
21
22. Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho
kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa
ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika
nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza
katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi
Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi
la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.
22
Sura Nyingine | Faharasa |