2.Sura Al-Baqara |
Imeshuka Madina | Ina aya 286 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Alif Lam Mim.
1
2. Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake;
ni uwongofu kwa wachamungu,
2
3. Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na
hutoa katika tuliyo wapa.3
4. Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako,
na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.
4
5. Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao
Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.
5
6. Hakika wale walio kufuru ni sawa kwao ukiwaonya
au usiwaonye, hawaamini.
6
7. Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao
na juu ya masikio yao, na juu ya macho yao pana kifuniko. Basi watapata
adhabu kubwa.
7
8. Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini.
8
9. Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale
walio amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui.
9
10. Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu
amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema
kwao uwongo.
10
11. Na wanapo ambiwa:Msifanye uharibifu ulimwenguni.
Husema: Bali sisi ni watengenezaji.
11
12. Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.
12
3. Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini
watu. Husema: Tuamini kama walivyo amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu,
lakini hawajui tu.
13
14. Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini.
Na wanapo kuwa peke yao na mashet'ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja
nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu.
14
15. Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawawacha
katika upotofu wao wakitangatanga ovyo.
15
16. Hao ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu;
lakini biashara yao haikupata tija, wala hawakuwa wenye kuongoka.
16
17. Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto,
na ulipo tanda mwangaza wake kote kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao
na akawawacha katika giza, hawaoni.
17
18. Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.
18
19. Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina
giza na radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili
ya mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.
19
20. Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila
ukiwatolea mwangaza huenda, na unapo wafanyia giza husimama. Na angelitaka
Mwenyezi Mungu angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu.
20
21. Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye
kuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.
21
22. Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii
ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa, na akateremsha maji kutoka
mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi
Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua.
22
23. Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia
mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu
badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.
23
24. Na mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe -
basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao
kanusha.
24
25. Na wabashirie walio amini na wakatenda mema
kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watapo pewa matunda
humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo pewa mbele. Na wataletewa matunda
yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio takasika; na wao humo watadumu.
25
26. Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano
hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba
hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema:
Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza
wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu,
26
27. Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada
ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na
wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara.
27
28. Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa
wafu akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?.
28
29. Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo
katika ardhi. Tena akazielekea mbingu, na akazifanya mbingu saba. Naye
ndiye Mjuzi wa kila kitu.
29
30. Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika:
Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo
atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa
sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua
msiyo yajua.
30
31. Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote,
kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi
ikiwa mnasema kweli.
31
32. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna
ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye
hikima.
32
33. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi
alipo waambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri
za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa
mnayaficha?
33
34. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam,
wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika
makafiri.
34
35. Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika
Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti
huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu.
35
36. Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili
na akawatoa katika waliyo kuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui
nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.
36
37. Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi,
na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali
toba na Mwenye kurehemu.
37
38. Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni
uwongofu utokao kwangu, basi watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa
khofu juu yao wala hawatahuzunika.
38
39. Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu,
hao ndio watakao kuwa watu wa Motoni, humo watadumu.
39
40. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu
niliyo kuneemesheni, na timizeni ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi
yenu, na niogopeni Mimi tu.
40
41. Na aminini niliyo yateremsha ambayo yanasadikisha
mliyo nayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa
thamani ndogo. Na niogopeni Mimi tu.
41
42. Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha
kweli nanyi mnajua.
42
43. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na inameni
pamoja na wanao inama.
43
44. Je! Mnawaamrisha watu mema na mnajisahau nafsi
zenu, na hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je, hamzingatii?
44
45. Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali;
na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu,
45
46. Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na
Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika watarejea kwake.
46
47. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni zile neema
zangu nilizo kuneemesheni, na nikakuteuweni kuliko wote wengineo.
47
48. Na iogopeni Siku ambayo mtu hatomfaa mtu kwa
lolote, wala hayatakubaliwa kwake maombezi, wala hakitapokewa kikomboleo
kwake; wala hawatanusuriwa.
48
49. Na vile tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni
walio kupeni adhabu mbaya, wakiwachinja wana wenu wa kiume na wakawawacha
hai wanawake; na katika hayo ulikuwa ni mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola
wenu Mlezi.
49
50. Na tulipo ipasua bahari kwa ajili yenu na
tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa Firauni, na huku mnatazama.
50
51. Na tulipo muahidi Musa masiku arubaini, kisha
mkachukua ndama (mkamuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
51
52. Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate
kushukuru.
52
53. Na tulipo mpa Musa Kitabu na pambanuo ili
mpate kuongoka.
53
54. Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu
wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu).
Basi tubuni kwa Muumba wenu na ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele
ya Muumba wenu. Naye akapokea toba yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba
na Mwenye kurehemu.
54
55. Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka
tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia.
55
56. Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili
mpate kushukuru.
56
57. Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni
Manna na Salwa; tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyo kuruzukuni.
Nao hawakutudhulumu Sisi lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao.
57
58. Na tulipo sema: Ingieni mji huu, na humo mle
mpendapo maridhawa, na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni:
Tusamehe! Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
58
59. Lakini walio dhulumu waliibadili kauli isiyo
kuwa waliyo ambiwa. Kwa hivyo tukaiteremsha juu ya wale walio dhulumu adhabu
kutoka mbinguni kwa sababu ya walivyo kuwa wamepotoka.
59
60. Na Musa alipo omba maji kwa ajili ya watu
wake, tulimwambia: Lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatimbuka chemchem
kumi na mbili; kila kabila ikajua mahali pake pa kunywea. Tukawaambia:
Kuleni na mnywe riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msiasi katika nchi mkafanya
uharibifu.
60
61. Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia
chakula cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile
vinavyo mea katika ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake,
na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho
bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo viomba. Na wakapigwa na unyonge,na
umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu
walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo
haki. Hayo ni kwa walivyo asi na wakapindukia mipaka.
61
62. Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo,
na Wasabai; yeyote atakaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na
akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa
khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
62
63. Na tulipo chukua ahadi yenu, na tukaunyanyua
mlima juu yenu (tukakwambieni): Shikeni kwa nguvu haya tuliyo kupeni, na
yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kujilinda.
63
64. Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa
si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema zake, mngeli kuwa miongoni
mwa wenye kukhasirika.
64
65. Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni
mwenu walio ivunja Sabato,(siku ya mapumziko, Jumaa Mosi) na tukawaambia:
Kuweni manyani wadhalilifu.
65
66. Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale
walio kuwa katika zama zao na walio kuja baada yao, na mawaidha kwa wachamngu.
66
67. Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi
Mungu anakuamrisheni mchinje ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha?
Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa
wajinga.
67
68. Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie
ni ng'ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng'ombe huyo si mpevu,
wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.
68
69. Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie
nini rangi yake? Akasema: Yeye anasema, kuwa ng'ombe huyo ni wa manjano,
na rangi yake imekoza, huwapendeza wanao mtazama.
69
70. Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie
ni yupi? Hakika tunaona ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah,
Mwenyezi Mungu akipenda, tutaongoka.
70
71. Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni ng'ombe
asiye tiwa kazini kulima ardhi wala kumwagia maji mimea, mzima, hana baka.
Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye
hayo.
71
72. Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana
kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha.
72
73. Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo
ng'ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni
Ishara zake ili mpate kufahamu.
73
74. Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo,
hata zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani kuna mawe yanayo timbuka mito,
na kuna mengine yanayo pasuka yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine
huanguka kwa sababu ya khofu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye
kughafilika na mnayo yafanya.
74
75. Mnatumai watakuaminini na hali baadhi yao
walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha wakayabadili baada ya
kuwa wameyafahamu, na hali wanajua?
75
76. Na wanapo kutana na wale walio amini husema:
Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao, wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyo
kufunulieni Mwenyezi Mungu ili wapate kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi?
Basi hamfahamu nyinyi?
76
77. Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua
wanayo yaficha na wanayo yatangaza?
77
78. Na wako miongoni mwao wasio jua kusoma; hawakijui
Kitabu isipo kuwa uwongo wanao utamani, nao hawana ila ni kudhania tu.
78
79. Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono
yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho
pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo andika mikono yao, na ole wao kwa
yale wanayo yachuma.
79
80. Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku
chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu
hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo
msiyo yajua?
80
81. Naam, anaye chuma ubaya - na makosa yake yakamzunguka
hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
81
82. Na wale walio amini na wakatenda mema, hao
ndio watu wa Peponi, humo watadumu.
82
83. Na tulipo funga agano na Wana wa Israili:
Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa
na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na
toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi
mnapuuza.
83
84. Na tulipo chukua agano lenu kuwa hamtamwaga
damu zenu, wala hamtatoana majumbani mwenu; nanyi mkakubali nanyi mnashuhudia.
84
85. Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa
baadhi yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni
mateka mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya
Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni
mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa
kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale
mnayo yatenda.
85
86. Hao ndio walio nunua uhai wa dunia kwa (uhai
wa) Akhera; kwa hivyo hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.
86
87. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha
baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo
waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni
Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha,
na wengine mkawauwa.
87
88. Na walisema: Nyoyo zetu zimefunikwa. Bali
Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru zao: kwa hivyo ni kidogo tu wanayo
yaamini.
88
89. Na kilipo wajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi
Mungu kinacho thibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi
kuwashinda makafiri - yalipo wajia yale waliyo kuwa wakiyajua waliyakanusha.
Basi laana ya Mwenyezi Mungu juu ya wakanushao!
89
90. Kiovu kweli walicho jiuzia nafsi zao, nacho
ni kule kukataa kwao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kuona
maya kwa kuwa Mwenyezi Mungu humteremshia fadhila yake amtakaye miongoni
mwa waja wake. Basi wamejiletea wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu. Na makafiri
watapata mateso ya kudhalilisha.
90
91. Na wanapo ambiwa: Yaaminini aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu. Wao husema: Tunaamini tuliyo teremshiwa sisi. Na huyakataa
yasiyo kuwa hayo. Na hali ya kuwa hii ndiyo Haki inayo thibitisha yale
waliyo nayo wao. Sema: Mbona mliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani
ikiwa kweli mlikuwa Waumini?
91
92. Na alikufikieni Musa na hoja zilizo waziwazi,
kisha mkamchukua ndama (kumuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
92
93. Na tulipo chukua ahadi yenu na tukauinua mlima
juu yenu (tukakwambieni): Kamateni kwa nguvu haya tuliyo kupeni na sikieni.
Wakasema: Tumesikia na tumekataa! Na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya)
ndama kwa kufuru yao. Sema: Ni uovu mno iliyo kuamrisheni imani yenu ikiwa
ni wenye kuamini.
93
94. Sema: Ikiwa nyumba ya Akhera iliyoko kwa Mwenyezi
Mungu ni yenu tu bila ya watu wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi
mnasema kweli.
94
95. Wala hawatayatamani kamwe kwa sababu ya yale
yaliyo tangulizwa na mikono yao; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema
wanao dhulumu.
95
96. Na hakika utawaona ni wenye kuwashinda watu
wote kwa pupa ya kuishi, na kuliko washirikina. Kila mmoja wao anatamani
lau angeli pewa umri wa miaka elfu. Wala hayo ya kuzidishiwa umri hayamuondoshei
adhabu; na Mwenyezi Mungu anayaona wanayo yatenda.
96
97. Sema: Aliye kuwa ni adui wa Jibril, basi huyo
ndiye aliye iteremsha Qur'ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu
inayo thibitisha yaliyo kuwa kabla yake, na ni uwongofu na bishara njema
kwa Waumini.
97
98. Aliye kuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika
wake na Mitume wake na Jibril na Mikail, basi hakika Mwenyezi Mungu ni
adui wa makafiri.
98
99. Hakika tumekuteremshia Ishara zilizo wazi
na hapana wanao zikataa ila wapotovu.
99
100. Je! Ati ndio kila wanapo funga ahadi huwapo
kikundi miongoni mwao kikaivunja? Bali wengi wao hawaamini.
100
101. Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale
walio pewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo
yao kama kwamba hawajui.
101
102. Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani
kuuzulia ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani
ndio walio kufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa
Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha
yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza
kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru
mtu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatayo wadhuru wala hayawanufaishi.
Na hakika wanajua kwamba aliye khiari haya hatakuwa na fungu lolote katika
Akhera. Na hakika ni kiovu mno walicho jiuzia nafsi zao laiti wangelijua.
102
103. Na lau kuwa wangeamini na wakaogopa, bila
ya shaka malipo yatokayo kwa Mwenyezi Mungu yange kuwa bora. Laiti wangeli
kuwa wanajua!
103
104. Enyi mlio amini! Msiseme: "Raa'ina", na
semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
104
105. Walio kufuru miongoni mwa watu wa Kitabu
na washirikina hawapendi mteremshiwe kheri yoyote kutoka kwa Mola wenu
Mlezi. Na Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi
Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
105
106. Ishara yoyote tunayo ifuta au tunayo isahaulisha
tunailetea iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu?
106
107. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa
mbingu na ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
107
108. Au mnataka kumwomba Mtume wenu kama alivyo
ombwa Musa zamani? Na anaye badilisha Imani kwa ukafiri bila ya shaka huyo
ameipotea njia iliyo sawa.
108
109. Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani
lau wange kurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa
ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia
Haki. Basi sameheni na wachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atapo leta
amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
109
110. Na shikeni Sala na toeni Zaka; na kheri
mtakazo jitangulizia nafsi zenu mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu anayaona mnayo yafanya.
110
111. Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa
Yahudi au Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama
nyinyi ni wasema kweli.
111
112. Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake
kwa Mwenyezi Mungu naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake
Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
112
113. Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao
jambo. Na Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo. Na ilhali wote wanasoma
Kitabu hicho hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasio jua kitu
mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya
Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitilafiana.
113
114. Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye
zuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake na akajitahidi
kuiharibu? Watu hao haitawafalia kuingia humo ila nao wanaogopa. Duniani
watapata hizaya na Akhera watapata adhabu kubwa.
114
115. Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi
Mungu. Basi kokote mnako elekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi
Mungu ni mwenye wasaa na Mjuzi.
115
116. Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana.
Subhanahu! Ametakasika na hayo. Bali vyote viliomo mbinguni na duniani
ni vyake. Vyote vinamt'ii Yeye.
116
117. Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina
ruwaza; na anapo taka jambo basi huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.
117
118. Na walisema wale wasio jua kitu: Mbona Mwenyezi
Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale walio
kuwa kabla yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi
tumeziweka wazi Ishara kwa watu wenye yakini.
118
119. Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri,
na mwonyaji. Na wala hutaulizwa juu ya watu wa Motoni.
119
120. Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo,
mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu.
Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata
mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.
120
121. Wale tulio wapa Kitabu, wakakisoma kama
ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini. Na wanao kikataa basi hao
ndio wenye kukhasiri.
121
122. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu
niliyo kuneemesheni, na hakika Mimi nikakufadhilisheni kuliko wengineo
wote.
122
123. Na iogopeni siku ambayo hatamfaa mtu mwenziwe
kwa lolote, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo, wala maombezi hayatamfaa,
wala hawatanusuriwa.
123
124. Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim
kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya
uwe mwongozi wa watu. Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema:
Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu.
124
125. Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya
Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipo kuwa
akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na
Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu
na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na kusujudu.
125
126. Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi!
Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao
muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia
nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo
ni pahala pabaya mno pa kurejea.
126
127. Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua
misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tutakabalie! Hakika
Wewe ndiye Msikizi Mjuzi.
127
128. Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye
kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu
kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
128
129. Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye
tokana na wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase.
Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
129
130. Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipo
kuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini Sisi tulimteuwa
yeye katika dunia; na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu
wema.
130
131. Na Mola wake Mlezi alipo mwambia: Silimu,
Nyenyekea! Alinena: Nimesilimu, nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu wote.
131
132. Na Ibrahim akawausia wanawe, na pia Yaaqub:
Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteulieni Dini hii; basi msife
ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.
132
133. Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti,
akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu
wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is- hak, Mungu Mmoja tu,
na sisi tunasilimu kwake.
133
134. Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata
waliyo yachuma, nanyi mtapata mtakayo yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi
waliyo kuwa wakiyafanya wao.
134
135. Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo
ndio mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa
katika washirikina.
135
136. Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu
na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail
na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia
waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina
ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.
136
137. Basi wakiamini kama mnavyo amini nyinyi,
itakuwa kweli wameongoka. Na wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani
tu. Na Mwenyezi Mungu atakutosheni kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye
Msikizi, Mjuzi.
137
138. Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu,
na nani aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye
kumuabudu Yeye tu.
138
139. Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu,
naye ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu
na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.
139
140. Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak
na Yaakub na wajukuu zao walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi
mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko
yule aliye ficha ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi
Mungu si mwenye kughafilika na hayo myafanyayo.
140
141. Hao ni watu walio kwisha pita. Wao watapata
waliyo yachuma, na nyinyi mt apata mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi
yale waliyo kuwa wakifanya wao.
141
142. WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini
kilicho wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki
na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia
iliyo nyooka.
142
143. Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa
wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu.
Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata
Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo
gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu
na Mwenye kuwarehemu.
143
144. Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso
wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza
uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso
zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni
haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika
na yale wanayo yatenda.
144
145. Na hao walio pewa Kitabu, hata ukiwaletea
hoja za kila namna, hawatafuata Kibla chako; wala wewe hutafuata kibla
chao, wala baadhi yao hawatafuata kibla cha wengineo; na kama ukiyafuata
matamanio yao baada ya kukufikia ujuzi, hakika hapo utakuwa miongoni mwa
wenye kudhullumu.
145
146. Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama
wanavyo wajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali
wanajua.
146
147. Haki inatoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe
miongoni mwa wanao fanya shaka.
147
148. Na kila mmoja anao upande anao elekea. Basi
shindanieni mema. Popote mlipo Mwenyezi Mungu atakuleteni nyote pamoja.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
148
149. Na popote wendako elekeza uso wako kwenye
Msikiti Mtakatifu. Na hiyo ndiyo Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi
Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda.
149
150. Na popote wendako elekeza uso wako kwenye
Msikiti Mtakatifu. Na popote mlipo elekezeni nyuso zenu upande huo ili
watu wasiwe na hoja juu yenu, isipokuwa wale walio dhulumu miongoni mwao
Basi msiwaogope wao, lakini niogopeni Mimi - na ili nikutimizieni neema
yangu, na ili mpate kuongoka.
150
151. Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana
na nyinyi, anakusomeeni Aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu
na hikima na kukufundisheni mliyo kuwa hamyajui.
151
152. Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni
wala msinikufuru.
152
153. Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira
na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.
153
154. Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika
Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti; bali hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui.
154
155. Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya
khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao
subiri,
155
156. Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika
sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.
156
157. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa
Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.
157
158. Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika
alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya
Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye jitendea mwenyewe kheri basi
bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mjuzi.
158
159. Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha
nazo ni hoja zilizo wazi na uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa
watu Kitabuni -- hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye
kulaani.
159
160. Ila wale walio tubu na wakatengeneza na
wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba
na Mwenye kurehemu.
160
161. Hakika walio kufuru na wakafa hali ni makafiri,
hao iko juu yao laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.
161
162. Watadumu humo. Hawata-punguziwa adhabu wala
hawatapewa muda wa kupumzika.
162
163. Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana
mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
163
164. Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi,
na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa
viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni,
na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila
aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa
kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao
zingatia.
164
165. Na katika watu wapo wanao chukua waungu
wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini
walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana. Na laiti walio dhulumu
wakajua watakapo iona adhabu kuwa nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu na kuwa
Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!
165
166. Walio fuatwa watakapo wakataa wale walio
wafuata, na hali ya kuwa wamekwisha iona adhabu; na yatakatika mafungamano
yao.
166
167. Na watasema wale walio fuata: Laiti tungeweza
kurudi tukawakataa wao kama wanavyo tukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi
Mungu atakavyo waonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa
wenye kutoka Motoni.
167
168. Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi,
halali na vizuri, wala msifuate nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni adui
yenu aliye dhaahiri.
168
169. Yeye anakuamrisheni maovu na machafu, na
mumsingizie Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua.
169
170. Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu.
Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?
170
171. Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa
anaye mpigia kelele asiye sikia ila wito na sauti tu ni viziwi, mabubu,
vipofu, kwa hivyo hawaelewi.
171
172. Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni,
na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.
172
173. Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na
nyama ya nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye
kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala
kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
173
174. Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu katika Kitabu, wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni
mwao isipo kuwa moto, wala Mwenyezi Mungu hatawasemeza Siku ya Kiyama,
wala hatawatakasa. Nao watapata adhabu chungu.
174
175. Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu,
na adhabu badala ya maghfira. Ama wavumilivu wa Moto watu hawa!
175
176. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha
Kitabu kwa haki. Na wale walio khitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani
ulio mbali na haki.
176
177. Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande
wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa
kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na
katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza
ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati
wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.
177
178. Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi
katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na
mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe
kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana
na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya,
basi yeye atapata adhabu chungu.
178
179. Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi
enyi wenye akili, ili msalimike.
179
180. Mmeandikiwa -- mmoja wenu anapo fikwa na
mauti, kama akiacha mali -- afanye wasia kwa wazazi wake na jamaa zake
kwa namna nzuri inayo pendeza. Ni waajibu haya kwa wachamngu.
180
181. Na atakaye ubadilisha wasia baada ya kuusikia,
basi dhambi yake ni juu ya wale watakao ubadilisha; hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
181
182. Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo
au kupata dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
182
183. Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama
waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.
183
184. (Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na
atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu
katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini.
Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni
bora kwenu, kama mnajua.
184
185. Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo
Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi.
Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa
au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni
yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na
mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.
185
186. Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu,
waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba.
Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
186
187. Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana
na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu
anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba
yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni
Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri
katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike
nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu,
basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa
watu ili wapate kumcha.
187
188. Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na
kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi,
na hali mnajua.
188
189. Wanakuuliza khabarai ya miezi. Sema: Hiyo
ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kuziingia
nyumba kwa nyuma. Bali mwema ni mwenye kuchamngu. Na ingieni majumbani
kupitia milangoni. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
189
190. Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu
na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi
waanzao uadui.
190
191. Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe
popote walipo kutoeni; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane
nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi
nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
191
192. Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
192
193. Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na
Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila
kwa wenye kudhulumu.
193
194. Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na
vitu vitakatifu vimeekewa kisasi. Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni,
kwa kadiri alivyo kushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba
Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
194
195. Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu,
wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika
Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
195
196. Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu. Na ikiwa mkizuiwa,basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana.
Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na
atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya
kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama,
basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje
mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija
na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule
ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi
Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
196
197. Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia
kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye
vitendo vichafu wala asibishane katika Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya
Mwenyezi Mungu anaijua. Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi
ni uchamngu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili!
197
198. Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola
wenu Mlezi. Na mtakapo miminika kutoka A'rafat mtajeni Mwenyezi Mungu penye
Masha'ril Haram. Na mkumbukeni kama alivyo kuongoeni, ijapo kuwa zamani
mlikuwa miongoni mwa walio potea.
198
199. Kisha miminikeni kutoka pale wanapo miminika
watu, na muombeni Mwenyezi Mungu msamaha: hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
199
200. Na mkisha timiza ibada zenu basi mtajeni
Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na
wapo baadhi ya watu wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika
Akhera hana sehemu yoyote.
200
201. Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu
Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!
201
202. Hao ndio watakao pata sehemu yao kwa sababu
ya yale waliyo yachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
202
203. Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku
zinazo hisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea)
si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye
kumchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa
kwake.
203
204. Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake
kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu
kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu.
204
205. Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi
kwa kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi
ufisadi.
205
206. Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa
na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo
kwa mapumziko.
206
207. Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi
yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa
waja wake.
207
208. Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu
kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui
aliye wazi.
208
209. Na ikiwa mkateleza baada ya kukufikieni
hoja zilizo wazi, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye
hikima.
209
210. Je wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie
katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa?
Na kwa Mwenyezi Mungu ndio hurejeshwa mashauri yote.
200
211. Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara
ngapi zilizo wazi? Na anaye zibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia
basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
211
212. Walio kufuru wamepambiwa maisha ya duniani;
na wanawafanyia maskhara walio amini. Na wenye kuchamngu watakuwa juu yao
Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
212
213. Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi
Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha
Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana.
Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia
hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu
kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo
khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
213
214. Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni
kama yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara
na wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura
ya Mwenyezi Mungu itakuja? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.
214
215. Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayo
itoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na wasafiri.
Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua.
215
216. Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha
kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda
kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
216
217. Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika
mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini
kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye,
na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake
humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi
kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini
yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye
ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera.
Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
217
218. Hakika wale walio amini na wale walio hama
na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanao taraji rehema za
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
218
219. Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema:
Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake
ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho
chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri--
219
220. .--katika mambo ya dunia na mambo ya Akhera.
Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika
nao basi ni ndugu zenu; na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji.
Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
220
221. Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka
waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni.
Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa
mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia
kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini
yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka.
221
222. Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo
ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie
mpaka wat'ahirike. Wakisha t'ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda
wanao jisafisha.
222
223. Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni
konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni
Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara
njema Waumini.
223
224. Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika
viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha kuacha kufanya wema na kuchamngu na
kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye
kujua.
224
225. Mwenyezi Mungu hakushikeni kwa viapo vyenu
vya upuuzi. Bali anakushikeni kwa yanayo chuma nyoyo zenu. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
225
226. Kwa wanao apa kuwa watajitenga na wake zao,
wangojee miezi mine. Wakirejea basi Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye kusamehe
na Mwenye kurehemu.
226
227. Na wakiazimia kuwapa talaka basi, Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia na Mjuzi.
227
228. Na wanawake walio achwa wangoje peke yao
mpaka t'ahara (au hedhi) tatu zipite. Wala haiwajuzii kuficha alicho umba
Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na
Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo,
kama wakitaka kufanya sulhu. Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile
haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
228
229. T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa
wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho
wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana
na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana
na mipaka ya Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa.
Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka
ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhaalimu.
229
230. Na kama amempa t'alaka (ya tatu) basi si
halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi
hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi
Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayo ibainisha kwa watu wanao
jua.
230
231. Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia
kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala
msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu
nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni
neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu
na hikima anacho kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba
hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
231
232. Na mtakapo wapa wanawake t'alaka nao wakamaliza
eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana
kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anaye muamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi
Mungu anajua, lakini nyinyi hamjui.
232
233. Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto
wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya
baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi
mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe,
wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama
wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi
si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha
basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni
Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda.
233
234. Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha
wake, hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi. Na wanapo timiza
eda yao basi hapana ubaya kwao kwa wanao jifanyia kwa mujibu wa ada. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
234
235. Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa
kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu.
Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa
siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike
mwisho wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi
zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
na Mpole.
235
236. Hapana ubaya kwenu mkiwapa t'alaka wanawake
ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza,
mwenye wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza
kwa mujibu wa dasturi kuwa ni haki juu ya watendao mema.
236
237. Na mkiwapa t'alaka kabla ya kuwagusa, na
mmekwisha wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio
agana, isipo kuwa ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo
cha ndoa ki mikononi mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu
zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu
anayaona mnayo yatenda.
237
238. Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati,
na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
238
239. Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda
kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo kuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi
Mungu kama alivyo kufunzeni yale mliyo kuwa hamyajui.
239
240. Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakawacha
wake, na wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi kwa mwaka mmoja bila
ya kuwatoa nyumba. Na wanawake wenyewe wakiondoka, basi hapana ubaya kwenu
kwa waliyo jifanyia wenyewe kwa mujibu wa Sharia. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
240
241. Na wanawake walio achwa wapewe cha kuwaliwaza
kwa mujibu wa Sharia. Haya ni waajibu kwa wachamngu.
241
242. Namna hivi anakubainishieni Mwenyezi Mungu
Aya zake ili mpate kufahamu.
242
243. Hukuwaona wale walio toka majumbani kwao
kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha
akwahauisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini
wengi wa watu hawashukuru.
243
244. Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi na Mjuzi.
244
245. Ni nani atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu
mkopo mwema ili amzidishie mzidisho mwingi, na Mwenyezi Mungu hukunja na
hukunjua. Na Kwake Yeye mtarejea.
245
246. Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili
baada ya Musa, walipo mwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika
Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa
msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto wetu? Lakini walipo andikiwa
kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu
anawajua madhaalimu.
246
247. Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu
amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na
ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye,
naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu
yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu
humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.
247
248. Na Nabii wao akawaambia: Alama ya ufalme
wake ni kukuleteeni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu,
kitokacho kwa Mola wenu Mlezi, na mna mabaki ya waliyo yaacha kina Musa
na kina Harun, wanalichukua Malaika. Bila shaka katika hayo zimo dalili
kwenu ikiwa nyinyi mnaamini.
248
249.Basi Taluti alipo ondoka na majeshi alisema:
Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami,
na asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila atakaye teka kiasi ya kitanga
cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa wachache tu miongoni
mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja naye, walisema: Leo
hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini
ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi
makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye
kusubiri.
249
250. Na walipo toka kupambana na Jaluti na majeshi
yake walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu
yetu, na utusaidie tuwashinde watu Makafiri--
250
251. .--Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua,
na Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima,
na akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi
watu kwa watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye
fadhila juu ya walimwengu wote.
251
252. Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea
kwa haki. Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.
252
253. MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya
wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine
akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na
tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli
pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana.
Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau
kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda
atakavyo.
253
254. Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni
kabla haijafika Siku ambayo hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi.
Na makafiri ndio madhaalimu.
254
255. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye
hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake
pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele
yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao;
wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo
mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda
hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu.
255
256. Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu
umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini
Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
256
257. Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini.
Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao
ni Mashet'ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu
wa Motoni, na humo watadumu.
257
258. Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim
juu ya Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim
alipo sema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema:
Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha
jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye
kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
258
259. Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio
kwisha kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada
ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha
akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku
moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia
chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako.
Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi
tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena:
Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
259
260. Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi!
Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini?
Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane
na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete,
watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye
nguvu, na Mwenye hikima.
260
261. Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia
ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba.
Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye,
na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.
261
262. Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi
Mungu, kisha hawafuatishii masimbulizi wala udhia kwa walicho toa, wana
ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
262
263. Kauli njema na usamehevu ni bora kuliko
sadaka inayo fuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha
na Mpole.
263
264. Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa
masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala
hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano
wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha
tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu makafiri.
264
265. Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa
kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano
wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake
mardufu; na hata kama haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na
Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
265
266. Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na
kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata
mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa
na kimbunga chenye moto, kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni
Ishara ili mpate kufikiri.
266
267. Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri
mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie
kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba
macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.
267
268. Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na
anakuamrisheni mambo machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na
fadhila zitokazo kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
268
269. Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa
hikima bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.
269
270. Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo
weka basi hakika Mwenyezi Mungu anajua. Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
270
271. Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha
mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni
baadhi ya maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
271
272. Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi
Mungu humwongoa amtakaye. Na kheri yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu.
Wala msitoe ila kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote
mtakayo toa mtalipwa kwa ukamilifu, wala hamtadhulumiwa.
272
273. Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia
za Mwenyezi Mungu, wasio weza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye
wajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao.
Utawatambua kwa alama zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri
yoyote mnayo toa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.
273
274. Wale wanao toa mali zao usiku na mchana,
kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa
khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
274
275. Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo
simama aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema:
Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na
ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake
Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake
yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni,
humo watadumu.
275
276. Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na
huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae
dhambi.
276
277. Hakika wale walio amini na wakatenda mema
na wakashika Sala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao
Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
277
278. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu,
na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini.
278
279. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi
Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu
wala msidhulumiwe.
279
280. Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai)
angoje mpaka afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora
kwenu, ikiwa mnajua.
280
281. Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa
Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.
281
282. Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa
muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu,
wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu.
Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake
Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni
mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe
mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume
wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili
katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja
wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze
kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi
mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi
ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu,
basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi.
Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika
hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
wa kila kitu.
282
283. Na mkiwa safarini na hamkupata mwandishi,
yatosha kukabidhiwa rahani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe basi
aliye aminiwa airudishe amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola
wake Mlezi. Wala msifiche ushahidi. Na atakaye ficha basi hakika moyo wake
ni wenye kutenda dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
283
284. Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya
Mwenyezi Mungu. Na mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha,
Mwenyezi Mungu atakuhisabuni kwayo. Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu
amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
284
285. Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka
kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu,
na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya
yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet'ii.
Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.
285
286. Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote
ila kwa kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara
ya iliyo yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie
tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha
wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na
utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe
ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri.
286
Sura Nyingine | Faharasa |