Maelezo: Suuratul Baqara |
(1) Katika Aya hii ipo sehemu ya kuonesha muujiza wa Qur'ani Tukufu: nayo ni kauli yake Mtukufu "mbingu kama paa". Haya asingeyajua Nabii asiyejua kusoma ila kwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu, nayo ni kuwa mbingu kwa kisayansi ni kila kilicho izunguka dunia pande zote, na kwa ukomo wowote, na kwa sura yoyote katika anga, mpaka huko juu kabisa kwenye sayari nyenginezo, zilizoenea zisio na mwisho. Zote hizo zinazunguka kwa mpango wa ajabu, na sisi tunapata uvukuto na mn'gao wake, nazo zinakwenda kwa nguvu ya mvutano kama smaku. Katika sehemu ya mwanzo ya mbingu iliyo tuzunguka lipo anga linalo tukinga kama paa na mianga inayo dhuru kutokana na hizo sayari. Na tabaka hizo huachilia mianga yenye faida tu, ndipo penye mawingu yaletayo mvua. |
(1) Aya hii inaonyesha kuwa ahadi, au agano, ni waajibu wa pande zote mbili zilizo ahidiana kutimiza lilio lazimika. Akiacha mmojapo basi haimlazimu wa pili kutimiza agano lake. |
(1) ("Masiku" ni wingi wa Usiku. Wingi wa siku ni siku, kama ilivyo sahani, sabuni, silaha, sinia, sungura, saa. Ni makosa kwa Kiswahili kusema "masiku" kuwa ni wingi wa siku; "Masiku" ni wingi wa "Usiku". Kutumia "Masaa" kuwa ni wingi wa "Saa" ni makosa.) |
Kabla ya Uislamu zilikuwapo katika mji wa Madina kabila mbili za Kiarabu ambazo zilikuwa na uadui baina yao, nazo ni Aus na Khazraj. Na pia zilikuwako kabila za Kiyahudi nazo ni Banu Quraidha na Banu Nnadhir. Banu Quraidha walifungamana na Aus, na Banu Nnadhir walifungamana na Khazraj. Ilikuwa kabila mbili za Kiarabu zikipigana, zile kabila za Kiyahudi nazo huingia vitani, kila kabila upande wa rafiki zake, na zikiuwana na wenzao wa dini moja nao, na wakifukuzana makwao. Lakini kila moja katika kabila mbili hizo za Kiyahudi zikishughulika baadaye kuwakomboa mateka walio tekwa na rafiki zao wa Kiarabu. Wakiulizwa kwa nini mnawakomboa na hao walikuwa wakipigana nanyi upande wa maadui zenu? Wao wakisema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tuwakomboe mateka wa Kiyahudi. Na wanajifanya hawajui kama Mwenyezi Mungu amewaamrisha vile vile wasiuwane wala wasitoane majumbani mwao. Kwa hivyo ndio wanaamini sehemu ya Kitabu na wanaikataa nyengine. |
(1) (Mwenyezi Mungu alimwambia Musa: "Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe...mtu asiye sikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake." |
(1) Katika lugha ya Kiyahudi ya Kiebrania lipo neno "Rai'nu" ambalo limejengwa na neno "Ra'" kwa maana ya "Shari" na neno "nu" linaonesha jamii, wingi. Na maana ya neno lote ni kuwa "Wewe ni shari yetu", wakikusudia kumwambia Mtume hayo. |
(1) Wanasema wafasiri kuwa Mayahudi wanaelekea kwenye Mwamba katika Beitul Muqaddas na Wakristo wanaelekea Mashariki. |
(1) Qurani imeutangulia utibabu wa kisasa kwa kukataza kula mzoga, kwani kifacho kwa ukongwe au ugonjwa husabibishwa na sumu inayo mdhuru mlaji. Kadhaalika cha kunyongwa au maradhi huinajisi damu, na ndani yake huwamo vingi vya kudhuru kama jasho na mkojo. Na nguruwe husabibisha maradhi ya khatari kama TRICHINOSIS ambayo khatimaye huharibu moyo na mapafu na husabibisha mauti. |
(1) Hali ya dharura inaruhusisha kinacho harimishwa, kwa sababu mauti ya yakini yanashinda madhara yanayo weza kustahamilika, na kwamba mwenye kulazimika kwa dharura haimfalii kupindukia mpaka wa dharura, wala asikiuke kile alicho lazimika kukila. |
(1)Waarabu zama za jahiliya walikuwa hawafanyi usawa baina ya watukufu na wanyonge. Akiuliwa mwongozi hawatosheki na kumuuwa muuwaji bali huyo huachwa akenda kulipizwa kisasi kwa mwongozi wa kabila ya muuwaji. Kwao roho si sawa, na damu si sawa. Uislamu haukukubali haya, lakini ukapasisha Kisasi, roho kwa roho, mwenye kuuwa huuwawa. Muuwaji yeyote awaye atauliwa akiwa muungwana, mtumwa au mwanamke. Haya ni kwa ajili ya usawa katika damu; hapana mwenye damu tukufu na damu isiyo tukufu. Na inafahamika kwa ishara kuwa nafsi kwa nafsi. Na hii ni sharia ya milele, ilikuwako katika Taurat, na Injil na Qur'ani. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na tuliwaandikia kuwa nafsi kwa nafsi..." (taz. sura Almaida ). Na Mtume s.a.w. amesema: "Damu za Waislamu ni sawa." Na amesema: "Nafsi kwa nafsi". Zingatia: Uislamu kwa sharia ya kisasi ina nadhari nyengine, sio kama kanuni za kutungwa. Imewapa wenye kuuliwa mtu wao haki ya kutaka muuwaji auwawe, kuondoa fitna na umwagaji wa damu mkubwa. Imewapa haki ya kusamehe au kulipwa kisasi, wala haizuilii serikali kumfedhehi aliye uwa ikiona hivyo ni maslaha. Uislamu hauzingatii sababu ya kuuwa, kwani mwenye kuuwa amedhulumu hata ikiwa sababu gani. Na huenda ukitafuta sababu akaonewa huruma mkosa, na kumpuuza mkoswa. Na hayo hupelekea mchafuko wa watu kuchukua kisasi mkononi mwao, na kuzalikana makosa juu ya makosa ya kuuwa, kwa kutoridhika wale walio uliwa mtu wao. Nadharia hii ya Kiislamu sasa inadurusiwa katika vyuo vikuu vya Ulaya. |
(1) Imethibiti kwa matibabu ya kisasa kuwa Saumu kwa namna ya Qur'ani ina faida nyingi, katika hizo ni kuwa inasaidia katika kutibu maradhi ya sukari, inatengeneza matumbo, inapunguza maumivu ya viungo, na maradhi ya moyo, inapumzisha nyama za mwili, na inasafisha uchafu mwingi wenye madhara, na pia inakuwa ni kinga kwa maradhi mengi mengineyo. Je, vipi kwa mtu asiye jua kusoma na kuandika ayajue yote haya? |
(1) Uislamu unahisabu mwezi unapo andama na kugeuka sura kwa watu kupimia nyakati za ibada, na pia kwa mambo yao ya kidunia, kwa sababu hayo ni mambo ya kuonekana, na kwa hivyo taarikhi inajuulikana kwa sura ya mwezi. Mwezi kwa hakika ni kama kioo kinacho onyesha mwangaza wa jua huku duniani. Mwezi ukiwa kati baina ya jua na dunia hauonekani, na baadae mwezi mchanga unaandama na wakaazi wa dunia wanajua kuwa mwezi mpya umeanza. Ukifika mwezi katika upande unao kabiliana baina ya jua na dunia ndio unapo kuwa wakati wa mbaamwezi, mwezi mpevu. Khalafu unaendelea kupungua kama ulivyo kuwa kwanza ukizidi kukua. Kwa hivyo taarikhi inaanza tangu pale ulipo kuwa mwezi mchanga. Pale unapo onekana mwezi mchanga kama uzi ndio mwezi umeandama, huonekana upande wa magharibi, hata kwa dakika chache baada ya kuchwa jua nao hupotea. Hivyo hivyo siku baada ya siku huhisabiwa mpaka zipite siku 29 au 30. |
Aya 190 mpaka 195 zinaeleza sharia ya vita katika Uislamu. Nazo zinaeleza kwa matamshi yalio wazi haya yafuatayo: 1. Ruhusa ya kupigana imetolewa kwa ajili ya kujilinda na uvamizi wa vita wa vitendo khasa, au zikidhihiri dalili kuwa maadui wanataka vita. Vita havikulazimishwa kwa ajili ya vita wala kwa sababu ya kutaka kuwasilimisha watu kwa kuwauwa na kuwapiga vita. 2. Kunakatazwa kuvamia au kuanza uadui kwa njia yoyote ile. Basi hapana ruhusa kufanyiwa uadui asiye pigana, wala hapana ruhusa kuvuka mipaka ya uadui wakati wa vita: basi hauliwi asiye chukua silaha, wala hakhusiani na vita bali ni mwenye kukumbwa tu na vita. Wala hauliwi mwenye kusalimu amri na akatupa silaha. Wala hapana ruhusa kuwavunjia watu nyumba zao, huko ni kupita mpaka. 3. Mzingatie fadhila iliyo onyeshwa kwa kuamrishwa kuchamngu. Basi msivunje heshima ya wanawake kuwanajisi, hata washirikina wakifanya hayo. Wala msiwakatekate walio uwawa hata ikiwa makafiri wakiwafanyia hayo Waumini. Washirikina walimfanyia hayo Bwana wa Mashahidi, Hamza, wala Mtume s.a.w. hakutoa ruhusa kumfanyia hayo maiti yeyote, bali alikataza akasema:"Tahadharini msiwakatekate maiti". 4. Vita vinakwisha wakiacha washirikina kuwafitini Waumini katika Dini yao, na Dini inakuwa inataka akili na nyoyo zimwelekee Mwenyezi Mungu kwa uhuru. 5. Hapana vita katika mwezi mtukufu, nayo ni miezi ya Hija na Umra. Ikiwa washirikina watapigana katika miezi hiyo, basi Waumini nao yawapasa wapigane. 6. Kuacha kutoka kwenda pigana na maadui wanauwa pasina nasi kupigana nao ni kuipoteza kheri na wema. Kwa haya inadhihiri kuwa vita vya Islamu vina fadhila katika sababu zinazo pelekea kuanza kwake, na vina uadilifu katika kuviendesha. Viwapi hivi na vita vya mataifa mengine ya zamani na ya sasa! Vita vyao hao ni vya uchafu, na vita vya Islamu ni vya Haki na vyenye fadhila. > |
(1) Hayo mawe ni changarawe hutupwa mwahala maalumu katika Mina katika siku ya kuchinja (Idd) na siku tatu zifwatiazo. |
Maneno haya ya Qur'ani ni wito kwa Waumini wote iwe baina yao salama na amani, na yanafahamisha kuwa vita na khasama ni katika mwendo wa kumfuata Shetani. Waumini wote wanaitwa wawe katika hali ya salama na wengineo, na wao baina yao kwa wao, wasipigane na wengine wala wasipigane wenyewe kwa wenyewe.
Na maneno haya ya Qur'ani yanaonyesha kuwa mahusiano baina ya dola ya Kiislamu na nyenginezo ni salama, na huo ni msingi wa mwanzo wa dini zote za mbinguni. Wakati ilipo kuwa kanuni ya porini ndiyo inayo hukumu baina ya madola na kuwekea mipaka ya mahusiano yao, mwenye nguvu kumla mnyonge, Uislamu ulikuja na huu msingi wa kuamrisha kuwa mahusiano yawe ya Usalama. Pindi vikitokea vita basi viwe kwa ajili ya ulinzi na kuupinga uvamizi. Yaani ni kumlazimisha yule mwenye kufanya uadui awe mwenye usalama. Vita vilivyo ruhusiwa na Uislamu ni kuthibitisha nguzo za amani, na kuhakikisha uadilifu. Vita hivi ni vita vya salama, kwa ajili ya uadilifu na amani. |
(1) Zingatia: Khabari ya eda ya mt'alaka limefasiriwa neno "Qurui" na wanazuoni wengi kuwa ni "Hedhi". Na wamefasiri Shafii (na Malik) kuwa ni "T'ahara". Khabari nyengine za eda zitakuja baadae. Sharia ya eda imekuja ili kuhakikisha kuwa ipo mimba au hapana, kwani hayo hayawezi kuhakikishwa ila baada ya kupita hedhi (au t'ahara) tatu, kwani mbegu za uzazi haziwezi kuishi baada ya hedhi tatu. Mwenye mimba kwa kawaida hatoki hedhi, na akitoka ni mara moja au sana mara mbili. Kwani hakika hapo ile mimba huwa imepevuka kwa muda huo hata kufikia kujaza eneo lote la tumbo la uzazi, na kwa hivyo ikazuia kuteremka damu ya mwezi. Hiyo ni kudra ya Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake, na hayakuwa hayo yanajuulikana na Waarabu, na wala hayakuwa yajuulikaane na Nabii asiye jua kusoma. Lakini Mwenyezi Mungu alimteremshia Qur'ani, akamfunza yeye na akaufunza umma wake. Na sababu ya pili ya sharia ya eda ni kumpa fursa ya mt'alaka kurejea kwa mumewe baada ya kuwaza na kufikiri na kutua. Na hapo ni mume kusema: "Nimekurejea". Lakini hii itahisabiwa ni moja katika t'alaka tatu. |
(1) Qur'ani inawajibisha mama amnyonyeshe mwanawe na asinyonyeshwe na mwingine ila kwa dharura, kwani kunyonyesha yeye ni faida kwa mama na mtoto katika siha. Na kuachisha ziwa kuwe kwa taratibu, na yajuzu kabla ya kutimiza muda ikiwa siha ya mtoto inaruhusu hayo |
(1) Neno la Qur'ani "ardhi iliyo nyanyuka" linaashiria yaliyo vumbuliwa na ilimu za sayansi za kisasa, kuwa maji ya chini yanakuwa yako mbali na mizizi. Kwa hivyo mizizi haiozi na vijizizi vidogo vinapata kunyonya chakula kwa wasaa na pia kuvuta pumzi. Kwa hivyo mazao yanakuwa mema, kwa mvua ijayo au hata manyunyu. (Nasi twajua mikarafuu au minazi ya bondeni haina maisha wala haistawi.) |
Riba iliyo tajwa katika Aya hii ni riba ya kijahiliya, nayo ni ziada juu ya deni kwa sababu ya kuakhirisha kulipa. Hii ni haramu, ikiwa kidogo au nyingi. Amesema Imam Ahmad: Haimfalii Muislamu kukanya haya. Kinyume cha hayo ni faida ya biashara, na hii inathibitishwa na hadithi ya Mtume s.a.w.: Ngano kwa ngano, kama ile ile, mkono kwa mkono. Shairi kwa shairi, kama ile ile, mkono kwa mkono. Dhahabu kwa dhahabu, kama ile ile, mkono kwa mkono. Fedha kwa fedha, kama ile ile, mkono kwa mkono. Na tende kwa tende, kama ile ile, mkono kwa mkono. Mwenye kuzidisha au kutaka kuzidisha basi amekula riba. Wanazuoni wamewafikiana kuwa ni haramu kuzidisha katika kubadilishana kitu cha jinsi moja, na wameruhusu kuzidisha ikiwa vitu vya jinsi mbali mbali. Lakini wameharimisha kuakhirisha katika vitu vya namna hii. Na wamekhitalifiana katika kukisia vitu vingine khitilafu kubwa. Katika rai iliyo karibu mno ni kukisia kama haya kila kinacho liwa kinacho weza kuwekwa kisiharibike. Ama riba ya kijahiliya hapana khitilafu yoyote -- mwenye kukanya basi ni kaafiri.
Riba ya kijahiliya humtia dhiki na kiwewe mwenye kula na mwenye kuliwa, kwa wasiwasi na kumshughulisha akili kwa mali aliyo kopesha au aliyo kopa. Mwenye kukopa ana dhiki na kushughulika akili yake hata hawezi kushughulikia kazi yake, na mwenye kukopesha anakuwa na hamu na khofu kuwa hatolipwa. Na baadhi ya madaktari wanaona kuzidi kwa maradhi ya "presha" na moyo ni kwa sababu ya kuzidi riba. Na kuharimishwa riba na Qur'ani kunawafikiana na mafailasufi wa zamani, kama Aristotle alivyo sema kuwa uchumi wa riba si uchumi wa tabia, kwani pesa hazizai pesa. Wataalamu wa uchumi wamethibitisha kwamba njia za uchumi ni nne: Tatu katika hizo ni zenye kuzaa matunda, ama ya nne haizai kitu. Zenye kuzaa ni kibarua, tena inafuatia ufundi na ukulima na kujasirisha katika biashara, kwani katika hiyo ni kuhamisha bidhaa kutoka pahala zilipo undwa kuzipeleka pa kuzitumia, na hiyo kwa hakika imekuwa ni kuzalisha matunda. Ama njia ya nne ndiyo hiyo faida ya riba. Katika kukopesha hajitii mtu khasarani bali ni faida tu, na hapana kuzalisha matunda ila kwa kazi ya yule aliye kopeshwa. Faida yake ni kwa kiasi ya mkopo. Ikiwa sababu yenyewe ni mkopo mwenye kukopesha haingii khatarini kwa kuwa anayo dhamana. |