6.Suurat An'aam |
Imeshuka Makka | Ina aya 165 |
Utangulizi | Orodha ya Sura | Faharasa |
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0
1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi,
na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya
wengine sawa na Mola wao Mlezi.
1
2. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha akakuhukumieni ajali,
na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnatia shaka.
2
3. Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani
yenu na ya nje yenu. Na anajua mnayo yachuma.
3
4. Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za Mola wao Mlezi
ila wao huwa wenye kuipa nyongo.
4
5. Wameikanusha Haki ilipo wajia. Basi zitawajia khabari za yale
waliyo kuwa wakiyakejeli.
5
6. Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka
katika nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya
mito inapita chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha
baada yao kizazi kingine.
6
7. Na lau tungeli kuteremshia kitabu cha karatasi, wakakigusa kwa
mikono yao, wangeli sema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uchawi dhaahiri.
7
8. Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungeli teremsha
Malaika, basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo wasingeli
pewa muhula.
8
9. Na kama tungeli mfanya Malaika bila ya shaka tungeli mfanya kama
binaadamu, na tungeli watilia matatizo yale wanayo yatatiza wao.
9
10. Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa kejeli, lakini
walio wafanyia kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa wao wanayafanyia
kejeli.
10
11. Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa
wanao kanusha.
11
12. Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema:
Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika
atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe
hawaamini.
12
13. Na ni vyake vilio tulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia
na Mwenye kujua.
13
14. Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu,
ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi?
Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa
usiwe miongoni wa washirikina.
14
15. Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku kubwa hiyo ikiwa nitamuasi
Mola wangu Mlezi.
15
16. Siku hiyo yule atakaye epushwa nayo adhabu hiyo atakuwa Mwenyezi
Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio wazi.
16
17. Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa
kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye
Mwenye uweza wa kila kitu.
17
18. Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye Mwenye hikima
na Mwenye khabari zote.
18
19. Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu.
Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili
kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia
kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii
hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha.
19
20. Wale Tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto
wao. Wale walio zikhasiri nafsi zao hawaamini.
20
21. Na nani dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu,
na akazikanusha Ishara zake? Hakika madhaalimu hawafanikiwi.
21
22. Siku tutapo wakusanya wote pamoja, kisha tuwaambie walio shirikisha:
Wako wapi washirikishwa wenu mlio kuwa mnadai?
22
23. Kisha hautakuwa udhuru wao ila ni kusema: Wallahi! Mola wetu
Mlezi! Hatukuwa washirikina.
23
24. Tazama jinsi wanavyo jisemea uwongo wenyewe. Na yamewapotea waliyo
kuwa wakiyazua.
24
25. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza; na tumezitia pazia nyoyo
zao wasije kuyafahamu. Na upo uziwi masikioni mwao, na wakiona kila Ishara
hawaiamini. Hata wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema walio kufuru:
Hizi si chochote ila hadithi za watu wa kale.
25
26. Nao huwazuia watu, na wao wenyewe wanajitenga nayo. Nao hawaangamizi
ila nafsi zao tu, wala wao hawatambui.
26
27. Na unge ona watakapo simamishwa kwenye Moto, wakawa wanasema:
Laiti tungeli rudishwa, wala hatutakanusha tena Ishara za Mola wetu Mlezi,
na tutakuwa miongoni wa Waumini.
27
28. Bali yamewadhihirikia waliyo kuwa wakiyaficha zamani. Na kama
wangeli rudishwa bila ya shaka wange yarejea yale yale waliyo katazwa.
Na hakika hao ni waongo.
28
29. Na walisema: Hakuna mengine ila maisha yetu haya ya duniani,
wala sisi hatutafufuliwa.
29
30. Na lau ungeli ona watavyo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi,
akawaambia: Je, si kweli haya? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola
Mlezi wetu ni kweli. Yeye atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile
mlivyo kuwa mnakataa.
30
31. Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu,
mpaka ilipo wajia Saa kwa ghafla, wakasema: Ole wetu kwa tuliyo yapuuza!
Nao watabeba mizigo yao juu ya migongo yao. Ni maovu hayo wanayo yabeba.
31
32. Na maisha ya dunia si chochte ila ni mchezo na pumbao tu. Na
hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanao mcha Mungu. Basi, je, hamtii
akilini?
32
33. Tunajua ya kwamba yanakuhuzunisha wanayo yasema. Basi hakika
wao hawakukanushi wewe, lakini hao madhaalimu wanazikataa Ishara za Mwenyezi
Mungu.
33
34. Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia
kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na hapana
wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia baadhi
ya khabari za Mitume hao.
34
35. Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza
kutafuta njia ya chini kwa chini ya ardhi, au ngazi kwendea mbinguni ili
uwaletee Ishara -- Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa angeli wakusanya
kwenye uwongofu. Basi usiwe miongoni mwa wasio jua.
35
36. Hakika wanao kubali ni wale wanao sikia. Na ama wafu Mwenyezi
Mungu atawafufua, na kisha kwake Yeye ndio watarejeshwa.
36
37. Hakika wanao kubali ni wale wanao sikia. Na ama wafu Mwenyezi
Mungu atawafufua, na kisha kwake Yeye ndio watarejeshwa.
37
38. Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka kwa mbawa
zake mbili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote.
Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa.
38
39. Na walio kanusha Ishara zetu ni viziwi na mabubu waliomo gizani.
Mwenyezi Mungu humwachia kupotea amtakaye, na humweka katika Njia iliyo
nyooka amtakaye.
39
40. Sema: Mwaonaje ikikujieni adhabu ya Mwenyezi Mungu, au ikakufikieni
hiyo Saa - mtamwomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni wakweli?
40
41. Bali Yeye ndiye mtakaye mwomba, naye atakuondoleeni mnacho mwombea
akipenda. Na mtasahau hao mnao wafanya washirika wake.
41
42. Na kwa yakini tulipeleka Mitume kwa kaumu zilizo kuwa kabla yako,
kisha tukazitia katika dhiki na mashaka ili zipate kunyenyekea.
42
43. Kwa nini wasinyenyekee ilipo wafika adhabu yetu? Lakini nyoyo
zao zilikuwa ngumu, na Shet'ani akawapambia waliyo kuwa wakiyafanya.
43
44. Basi walipo sahau walio kumbushwa tuliwafungulia milango ya kila
kitu. Mpaka walipo furahia yale waliyo pewa tuliwashika kwa ghafla, na
mara wakawa wenye kukata tamaa.
44
45. Ikakatwa mizizi ya watu walio dhulumu - na wa kuhimidiwa ni Mwenyezi
Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
45
46. Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu akanyakua kusikia kwenu, na kuona
kwenu, na akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu
ataye kuleteeni hayo tena? Angalia vipi tunavyo zieleza Ishara, kisha wao
wanapuuza.
46
47. Sema: Mwaonaje, ikikufikieni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla,
au kwa dhaahiri, jee wataangamizwa isipo kuwa walio dhulumu?
47
48. Na hatuwatumi Mitume ila huwa ni wabashiri na waonyaji. Na wenye
kuamini na wakatenda mema haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
48
49. Na walio kanusha Ishara zetu itawagusa adhabu kwa walivyo kuwa
wakipotoka.
49
50. Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu.
Wala sijui mambo yaliyo fichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika.
Mimi sifuati ila yanayo funuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa, kipofu
na mwenye kuona. Basi hamfikiri?
50
51. Na waonye kwayo wanao ogopa kuwa watakusanywa kwa Mola wao Mlezi,
hali kuwa hawana mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye, ili wapate kuchamngu.
51
52. Wala usiwafukuze wanao mwomba Mola Mlezi wao asubuhi na jioni
kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu
yako si juu yao hata kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye kudhulumu.
52
53. Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili waseme: Ni hao
ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu
hawajui wanao shukuru?
53
54. Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum!
Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye
fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea,
basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
54
55. Na ndio hivi tunavyo zieleza Ishara ili ibainike njia ya wakosefu.
55
56. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya Mwenyezi
Mungu. Sema: mimi sifuati matamanio yenu. Hivyo nitakuwa nimepotea, na
sitakuwa miongoni mwa walio ongoka.
56
57. Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu
Mlezi, nanyi mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana hukumu
ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu
kuliko wote.
57
58. Sema: Lau kuwa ninacho hicho mnacho kihimiza, ingeli kwisha katwa
shauri baina yangu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu anawashinda wote kuwajua
madhaalimu.
58
59. Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu.
Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua.
Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika
Kitabu kinacho bainisha.
59
60. Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho fanya mchana.
Kisha Yeye hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe. Kisha
kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya.
60
61. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake.
Na hukupelekeeni waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu
humfisha, nao hawafanyi taksiri.
61
62. Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki. Hakika,
hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu.
62
63. Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi kavu na baharini?
Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na haya
bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
63
64. Sema: Mwenyezi Mungu hukuokoeni kutoka hayo, na kutoka kila mashaka,
na kisha nyinyi mnamshirikisha!
64
65. Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu
au kutoka chini ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na kuwaonjesha
baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili wapate
kufahamu.
65
66. Na watu wako wameikanusha, nayo ni Haki. Sema: Mimi sikuwakilishwa
juu yenu.
66
67. Kila khabari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua.
67
68. Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka
waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi baada
ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu.
68
69. Wala wamchao Mungu hawana jukumu lolote kwao, lakini ni kukumbusha,
asaa wapate kujiepusha.
69
70. Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na pumbao, na
uhai wa dunia ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi ikaangamizwa
kwa sababu ya iliyo yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila Mwenyezi
Mungu. Na ingatoa kila fidia haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa kwa
sababu ya yale waliyo yachuma. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa,
na adhabu chungu.
70
71. Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae hatufai wala
hatudhuru, na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi? Tuwe
kama ambao mashet'ani wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki
wanao mwita ende kwenye uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika
uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa
Mola Mlezi wa viumbe vyote,
71
72. Na mshike Sala, na mcheni Yeye, na kwake Yeye ndiko mtako kusanywa.
72
73. aye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na anaposema:
Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku litapo
pulizwa barugumu, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye
Mwenye hikima na Mwenye khabari.
73
74. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu
kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu
ulio wazi.
74
75. Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi,
na ili awe miongoni mwa wenye yakini.
75
76. Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola
Mlezi wangu. Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua.
76
77. Alipo uona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu.
Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu
walio potea.
77
78. Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi
wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi
simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina.
78
79. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliye ziumba
mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina.
79
80. Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi
Mungu, na hali Yeye ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha naye,
ila Mola wangu Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya
kila kitu. Basi je, hamkumbuki?
80
81. Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu
kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia
uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata
amani, kama nyinyi mnajua?
81
82. Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma
- hao ndio watakao pata amani na wao ndio walio ongoka.
82
83. Na hizo ndizo hoja zetu tulizo mpa Ibrahim kuhojiana na watu
wake. Tunamnyanyua kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye
hikima na Mwenye ujuzi.
83
84. Na tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa.
Na Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman
na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wafanyao
wema.
84
85. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas. Wote walikuwa miongoni mwa
watu wema.
85
86. Na Ismail, na Al Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na wote tuliwafadhilisha
juu ya walimwengu wote.
86
87. Na kutokana na baba zao, na vizazi vyao na ndugu zao. Na tukawateuwa
na tukawaongoa kwenye Njia iliyo nyooka.
87
88. Hiyo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo humhidi amtakaye katika
waja wake. Na lau wangeli mshirikisha yangeli waharibikia waliyo kuwa wakiyatenda.
88
89. Hao ndio tulio wapa Vitabu na hukumu na Unabii. Ikiwa hawa watayakataa
hayo, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasio yakataa.
89
90. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewahidi. Basi fuata hidaya yao.
Sema: Mimi sikuombeni ujira. Haya hayakuwa ila ni mawaidha kwa walimwengu
wote.
90
91. Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri yake, walipo
sema: Mwenyezi Mungu hakumteremshia mwanaadamu chochote. Sema: Nani aliyo
teremsha Kitabu alicho kuja nacho Musa, chenye nuru na uwongofu kwa watu,
mlicho kifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha. Na mkafunzwa
mlio kuwa hamyajui nyinyi wala baba zenu? Sema: Mwenyezi Mungu. Kisha waache
wacheze katika porojo lao.
91
92. Na hiki ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa, chenye
kuhakikisha yaliyo tangulia, na ili uuwonye Mama wa Miji na walio pembezoni
mwake. Na wenye kuamini Akhera wanakiamini hichi, nao wanazihifadhi Sala
zao.
92
93. Nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzuliya uwongo Mwenyezi
Mungu, au anaye sema: Mimi nimeletewa wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote.
Na yule anaye sema: Nitateremsha kama alivyo teremsha Mwenyezi Mungu. Na
lau ungeli waona madhaalimu wanavyo kuwa katika mahangaiko ya mauti, na
Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa
adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu
yasiyo ya haki, na mlivyo kuwa mkizifanyia kiburi Ishara zake.
93
94. Nanyi mlitujia wapweke kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza.
Na mkayaacha nyuma yenu yote tuliyo kupeni, na wala hatuwaoni hao waombezi
wenu, ambao mlidai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu. Yamekatika
makhusiano baina yenu, na yamekupoteeni mliyo kuwa mkidai.
94
95. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa, zikachipua.
Humtoa aliye hai kutoka maiti, naye ni mtoaji maiti kutokana na aliye hai.
Huyo ndiye Mwenyezi Mungu. Basi vipi mnageuzwa?
95
96. Ndiye anaye pambazua mwangaza wa asubuhi; na ameufanya usiku
kwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi kwenda kwa hisabu. Hayo ndiyo
makadirio ya Aliye tukuka Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi.
96
97. Na Yeye ndiye aliye kuwekeeni nyota ili mwongoke kwazo katika
kiza cha bara na bahari. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanao
jua.
97
98. Na Yeye ndiye aliye kuzalisheni kutokana na nafsi moja. Pako
pahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa
watu wanao fahamu.98
99. Na Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka mbinguni; na kwayo tunatoa
mimea ya kila kitu. Kutokana na baadhi yao tukatoa mimea ya majani, tukatoa
ndani yake punje zilizo pandana; na kutokana na mitende yakatoka kwenye
makole yake mashada yaliyo inama; na bustani za mizabibu na mizaituni,
na makomamanga, yaliyo fanana na yasiyo fanana. Angalieni matunda yake
yanapo zaa na yakawiva. Hakika katika hayo pana Ishara kwa watu wanao amini.
99
100. Bado wamemfanyia Mwenyezi Mungu majini kuwa washirika wake,
na hali Yeye ndiye aliye waumba. Na wakamzulia, bila ya ujuzi wowote, kuwa
ana wana wa kiume na wa kike. Subhanahu, Ametakasika na ametukuka juu ya
hayo wanayo mbandikiza nayo!
100
101. Yeye ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ya ruwaza. Itakuwaje
awe na mwana naye hakuwa na mke? Naye ndiye aliye umba kila kitu. Naye
ni Mwenye kujua kila kitu.
101
102. Huyo ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu, hapana mungu
ila Yeye, Muumba wa kila kitu. Basi muabuduni Yeye tu. Naye ni Mtegemewa
wa kila kitu.
102
103. Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi,
Mwenye khabari.
103
104. Zimekwisha kukujieni hoja wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi
anaye ona ni kwa faida yake mwenyewe, na anaye pofuka basi ni khasara yake.
Nami si mtunzaji wenu.
104
105. Na namna hivyo tunazisarifu Aya, na wao wakwambie: Umesoma.
Na ili tuyabainishe kwa watu wanao jua.
105
106. Fuata uliyo funuliwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Hapana mungu
ila Yeye. Na jitenge na washirikina.
106
107. Na lau Mwenyezi Mungu angeli penda, wasingeli shiriki. Na Sisi
hatukukufanya wewe uwe mtunzaji wao. Wala wewe si mlinzi juu yao.
107
108. Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu,
wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna
hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa
Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda.
108
109. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa
ikiwafikia Ishara wataiamini. Sema: Ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na
nyinyi hamjui kuwa zitapo kuja hawato amini.
109
110. Nasi twazigeuza nyoyo zao na macho yao. Kama walivyo kuwa hawakuamini
mara ya kwanza, tunawaacha katika maasi yao wakitangatanga.
110
111. NA LAU kuwa tungeli wateremshia Malaika, na maiti wakazungumza
nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, bado wasingeli amini, ila Mwenyezi
Mungu atake. Lakini wengi wao wamo ujingani.
111
112. Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashet'ani wa kiwatu,
na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba-pamba, kwa udanganyifu.
Na angeli penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya hayo. Basi waache na wanayo
yazua.
112
113. Na ili nyoyo za wasio amini Akhera zielekee hayo, nao wayaridhie
na wayachume wanayo yachuma.
113
114. Je, nimtafute hakimu ghairi ya Mwenyezi Mungu, naye ndiye aliye
kuteremshieni Kitabu kilicho elezwa waziwazi? Na hao tulio wapa Kitabu
wanajua ya kwamba kimeteremshwa na Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi usiwe
katika wanao tia shaka.
114
115. Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu.
Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia
na Mwenye kujua.
115
116. Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza
na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila
ni wenye kusema uwongo tu.
116
117. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio
potea Njia yake, na ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio hidika.
117
118. Basi kuleni katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu, ikiwa
mnaziamini Aya zake.
118
119. Na kwa nini msile katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu,
naye amekwisha kubainishieni alivyo kuharimishieni, isipo kuwa vile mnavyo
lazimishwa? Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya kuwa na
ilimu. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua wanao pindukia
mipaka.
119
120. Na acheni dhambi zilizo dhaahiri na zilizo fichikana. Hakika
wanao chuma dhambi watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
120
121. Wala msile katika wale wasio somewa jina la Mwenyezi Mungu.
Kwani huo ni upotofu. Na kwa yakini mashet'ani wanawafunza marafiki zao
kubishana nanyi. Na mkiwafuata basi hapana shaka nyinyi mtakuwa washirikina.
121
122. Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru
inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani akawa hata
hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa wakiyafanya.
122
123. Kadhaalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa wakosefu
wao wafanye vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa nafsi
zao, nao hawatambui.
123
124. Na inapo wajia Ishara, wao husema: Hatutoamini mpaka tupewe
mfano wa walio pewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi
kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao walio kosa udhalili
na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo
kuwa wakivifanya.
124
125. Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi humfungulia
kifua chake kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake kina
dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu
anajaalia uchafu juu ya wasio amini.
125
126. Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka. Tumezipambanua
Aya kwa watu wanao kumbuka.
126
127. Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye
Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda.
127
128. Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi makundi ya majini!
Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na marafiki zao
katika wanaadamu waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Na
tumefikia ukomo wetu ulio tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto ndio
makaazi yenu, mtadumu humo, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako
Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua.
128
129. Ndio kama hivi tunawaelekeza madhaalimu wapendane wao kwa wao
kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma.
129
130. Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni Mitume kutokana
na nyinyi wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni mkutano
wa Siku yenu hii. Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na yaliwadanganya
maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri.
130
131. Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa wa kuiangamiza
miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika.
131
132. Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale waliyo yatenda.
Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
132
133. Na Mola wako Mlezi ndiye Mkwasi, Mwenye rehema. Akipenda atakuondoeni
na awaweke wengine awapendao badala yenu, kama vile alivyo kutoeni kutokana
na uzazi wa watu wengine.
133
134. Bila ya shaka hayo mnayo ahidiwa yatafika tu, wala nyinyi hamtaweza
kuyaepuka.
134
135. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezayo, na hakika mimi nafanya.
Mtakuja jua nani atakuwa na makaazi mema mwishoni. Hakika madhaalimu hawatafanikiwa.
135
136. Na wamemwekea sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea na wanyama
alio umba, nao husema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai yao
- na hii ni ya miungu tunao washirikisha. Basi vile walivyo wakusudia miungu
yao havimfikii Mwenyezi Mungu, na vilivyo kuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia
miungu yao. Ni uovu kabisa hayo wanayo yahukumu.
136
137. Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika washirikina
kuwauwa watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo wanayo
yazua.
137
138. Nao husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko. Hawatokula ila
wale tuwapendao - kwa madai yao tu. Na wanyama hawa imeharimishwa migongo
yao kupandwa. Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu
yao. Wanamzulia uwongo tu Mwenyezi Mungu. Atawalipa kwa hayo wanayo mzulia.
138
139. Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya
wanaume wetu tu, na wameharimishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa nyamafu
basi wanashirikiana. Mwenyezi Mungu atawalipa kwa maelezo yao hayo. Hakika
Yeye ni Mwenye hikima, Mwenye kujua.
139
140. Hakika wamekhasirika wale ambao wamewauwa watoto wao kwa upumbavu
pasipo kujua, na wakaharimisha alivyo waruzuku Mwenyezi Mungu kwa kumzulia
Mwenyezi Mungu. Hakika wamepotea, wala hawakuwa wenye kuongoka.
140
141. Na Yeye ndiye aliye ziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja,
na zisio tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali, na mizaituni
na mikomamanga inayo fanana na isiyo fanana. Kuleni matunda yake inapo
zaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo.
Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo.
141
142. Na katika wanyama amekujaalieni wenye kubeba mizigo na kutoa
matandiko. Kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, wala msifuate
nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu dhaahiri.
142
143. Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika kondoo, na
wawili katika mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au majike
wawili, au waliomo matumboni mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu
ikiwa nyinyi mnasema kweli
143
144. .Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je,
ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni
mwa yote majike? Au, nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya?
Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo,
kwa ajili ya kuwapoteza watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi
watu madhaalimu.
144
145. Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa
kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au
nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa
jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila
ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
145
146. Na wale walio fuata dini ya Kiyahudi tumewaharimishia kila mwenye
kucha. Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi tumewaharimishia shahamu yao,
isipo kuwa ile iliyo beba migongo yao au matumbo yao, au iliyo gandamana
na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na bila ya shaka Sisi
ndio wasema kweli.
146
147. Wakikukanusha basi wewe sema: Mola Mlezi wenu ni Mwenye rehema
iliyo enea. Wala haizuiliki adhabu yake kwa watu wakhalifu.
147
148. Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu ange taka
tusingeli shiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu chochote.
Vivi hivi walikanusha walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu yetu.
Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala
hamsemi ila uwongo tu.
148
149. Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya kukata. Na kama
angeli penda angeli kuhidini nyote.
149
150. Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa Mwenyezi Mungu
ameharimisha hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja nao. Wala
usifuate matamanio ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini Akhera,
na ambao wanamlinganisha Mola Mlezi wao na wengine.
150
151. Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi.
Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni
wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni
nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayo onekana, na yanayo
fichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa,
ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini.
151
152. Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa,
mpaka afikilie utu-uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu. Sisi
hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo semeni kwa
uadilifu ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo
amekuusieni ili mpate kukumbuka.
152
153. Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni,
wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni
ili mpate kuchamngu.
153
154. Tena tulimpa Musa Kitabu kwa kumtimizia (neema) aliye fanya
wema, na kuwa ni maelezo ya kila kitu, na uwongofu na rehema, ili wapate
kuamini mkutano wao na Mola wao Mlezi.
154
155. Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa. Basi
kifuateni, na mchenimngu, ili mrehemewe.
155
156. Msije mkasema: Hakika mataifa mawili kabla yetu yameteremshiwa
Kitabu; na sisi tulikuwa hatuna khabari ya waliyo kuwa wakiyasoma.
156
157. Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungeli kuwa
waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu
Mlezi, na uwongofu, na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko
yule anaye kanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa
wanao jitenga na Ishara zetu adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga
kwao.
157
158. Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au awafikie Mola wako
Mlezi, au zifike baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku zitakapo fika
baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu,
ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake.
Sema: Ngojeni, nasi pia tunangoja.
158
159. Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna
ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu;
kisha atawaambia yale waliyo kuwa wakiyatenda.
159
160. Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya
hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa.
160
161. Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia
Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye
kuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
161
162. Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa
kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
162
163. Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni
wa kwanza wa Waislamu.
163
164. Sema: Je nitafute Mola Mlezi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na hali
Yeye ndiye Mola Mlezi wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake.
Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola
wenu Mlezi, naye atakuambieni mliyo kuwa mkikhitalifiana.
164
165. Naye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na amewanyanyua
baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa hayo
aliyo kupeni. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika
Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
165
Sura Nyingine | Faharasa |