Maelezo: Suuratul An-a'am |
(1) Aya hii tukufu ni ishara ya ubora wa kuumba, na ubora wa kuumba unaonyesha Umoja na Upweke wa Mwenye kuumba na utukufu wake. Kwani mbingu na nyota zake, na sayari zake, na jua, na mwezi - vyote hivyo ni ushahidi wa Umoja wake. Na ardhi na viliomo ndani yake, navyo ni wanyama, mimea na visio na uhai, na milima na mabonde, na rutuba na ukame, na viliomo chini ya ardhi maadeni magumu na yanayo tiririka, na bahari na viliomo ndani yake kama lulu na vilio hai - vyote hivyo vinaonyesha Umoja wa Mwenye kuumba. Na giza la kila namna, kama giza la jabali, na bahari, na mapango, na ukungu ulio funga moja kwa moja hata mtu akiutoa mkono wake anakaribia kuwa asiouone - pia vyote hivyo vinaonyesha ujuzi usio kuwa na mfano, wa kuanzisha kuumba, wa Mwenyezi Mungu Aliye viumba. Hali kadhaalika nuru, na sababu zake mbali mbali, kama nuru ya jua, na mwangaza wa mwezi, na mwangaza wa nyota ... vyote hivyo vinaonyesha uanzishaji wa Mwenyezi Mungu wa kuumba bila ya kiigizo. |
(1) Kauli hii inaashiria maana ambayo wenye ilimu za kisasa wanaitaja. Wenye ilimu za mambo ya kiroho wanasema kuwa roho zina mwili khafifu, mwembamba na mwepesi, mfano wa ng'amba. Nazo hazidhihiri wala hazionekani. Na hayumkiniki kuonekana roho ila zikivaa huo mwili. Na Malaika hawana kiwiliwili. Katika viumbe vyote vya kiroho Malaika ndio khafifu kabisa kushinda vyote. Na hayumkini kuonekana ila kwa sura ya mwili. Na huu mwili ndio unakuwa kama mwanaadamu. |
(1) Kauli hii inafahamisha kuwa kujua mambo ya ghaibu kuko kwa Mwenyezi Mungu, na funguo za hayo ziko kwake tu. Na mambo ya ghaibu ni mafungu mawili: Ghaibu Mut'laq ambayo hayumkini kutambulikana na akili, kama mambo yatakayo mfikia mtu katika mustakbali. Na Ghaib Nisbiy hizi ni siri za ulimwengu na viliomo ndani yake, na kuweza kuvitumia kwa maslaha ya watu. Ujuzi wa hayo huweza kughibu kwa vizazi kadhaa, kisha ukadhihiri.. Na funguo ya hizi pia ziko kwa Mwenyezi Mungu, humwezesha amtakaye katika waja wake wale wanao zama kuusoma ulimwengu. Na katika hayo ni haya ya uvumbuzi ambao tunauona anao ufikilia mwanaadamu kwa kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. |